Kurasa

Alhamisi, 2 Oktoba 2014

THELUTHI MBILI YA RASIMU YA KATIBA YAPATIKANA DODOMA

Bunge maalumu la Katiba limepitisha rasimu ya katiba iliyopendekezwa. Hatua hiyo imefikiwa baada ya kura za ndio zilizopigwa na wajumbe kufikia kiwango kinachostahili.
Ili katiba hiyo iliyopendekezwa ipite ilitakiwa kuungwa mkono na kura za ndio theluthi mbili( 2/3) kutoka Tanzania bara na theluthi mbili (2/3) za ndio kutoka Zanzibar.
Jumla ya wajumbe wote wa bunge hilo la Katiba ni 629, huku 419 wakitoka Tanzania bara na 210 kutoka Zanzibar.
Zoezi hilo la upigaji kura ambalo lilianza Septemba 29 mpaka Oktoba 2, siku matokeo yalipotangazwa, lilisusiwa na wabunge wa upinzani waliounda umoja wao uitwao UKAWA, kwa madai kuwa baadhi ya vipengele vya awali vilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopewa kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa mwananchi, vilikuwa vimeondolewa.
Kabla ya kupitishwa kwa rasimu hiyo, bunge hilo maalum la katiba lilikaa kama kamati kujadili mapendekezo katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba.
Baada ya kamati hizo za bunge hilo kutoa mapendekezo yao, kamati ya uandishi ilikuwa na jukumu la kuandika upya Ibara za Sura za Rasimu ya Katiba zilizojadiliwa na Bunge Maalum na hatimaye kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya kukamilisha kazi hiyo.
Hivyo, Kamati ya Uandishi ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko katika Rasimu ya Katiba yanakidhi matakwa na masharti ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014.
Hatma ya katiba hiyo itahitimishwa kwa kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa na wananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni