Kurasa

Jumapili, 21 Septemba 2014

WASIRA NAE ATANGAZA KUGOMBEA URAIS 2015

WAZIRI wa Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, amesema bado ana nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Kauli hiyo, aliitoa wakati akifanya mahojiano kwenye kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi kinachorushwa na Star Tv.
Itakumbukwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiliwaadhibu makada wake sita akiwemo Wassira, mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya kampeni za urais.
Katika kipindi cha jana, Wasira alisema licha ya kupewa adhabu na chama chake kwa kuanza kampeni mapema, bado hajafuta dhamira ya kuwania nafasi hiyo.
Alisema adhabu hiyo ya chama haimzuii kuwania nafasi hiyo, bali imelenga kuzuia makada wa chama hicho kufanya mambo kinyume na taratibu za chama.
“Nia ya kuwania urais bado ninayo, nitaendelea nayo kulingana na taratibu za chama, mimi ni mtu safi na nimeanza siasa tangu nikiwa na umri wa miaka 15,” alisema.
Wasira, aliulizwa swali na mtangazaji wa kipindi hicho atawezaje kugombea urais wakati Katiba inazuia mtu aliyeshatakiwa kwa jinai na yeye alishawahi kushtakiwa.
Waziri huyo alikiri kushtakiwa na Jaji Joseph Warioba katika kesi ya uchaguzi, lakini kesi hiyo ni ya madai na si jinai.
“Kesi zote uchaguzi ni za madai, mtu aliyeshtakiwa kwa madai hazimkoseshi mtu kuwania urais, kesi ya jinaI ndiyo yenye kutoa zuio hilo…..mimi nipo ‘clean’ kwa kuwa nilishtakiwa kwa madai,” alisema.
Alisema rushwa katika sekta mbalimbali ni hatari kwa maenedeleo ya taifa na mtu mmoja mmoja hivyo kila mtu anapaswa akichukie na kuipiga vita.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni