Kurasa

Jumamosi, 27 Septemba 2014

WABUNGE WA TANZANIA SIO HALALI BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI

Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), jana imesema uchaguzi wa wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki ni batili kutokana na kukiuka ibara ya 50 ya mkataba wa kuanzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Jaji Kiongozi, Jean Bosco-Butasi akiwa na majaji wengine wa mahakama hiyo, Isaac Lenaola na Jaji Faustine Ntezilyayo, walitoa uamuzi huo katika hukumu ya kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mmoja wa wagombea ubunge wa Eala kutoka Tanzania, Anthony Komu (Chadema).
Jaji Faustine Ntezilyayo, walitoa uamuzi huo katika hukumu ya kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mmoja wa wagombea ubunge wa Eala kutoka Tanzania, Anthony Komu (Chadema).
Katika hukumu hiyo ya kurasa 38, mahakama hiyo, imempa ushindi Komu katika hoja zake zote tatu na kutupilia mbali pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi hiyo na hivyo, kuitaka Serikali kulipa gharama za kesi hiyo.
Katika shauri hilo namba saba la mwaka 2012, katika madai yake ya msingi Komu alikuwa anapinga utaratibu uliotumika kupata wagombea wa Bunge la Eala kutoka Tanzania akidai ulikiuka Ibara ya 50 ya mkataba wa kuanzishwa kwa EAC inayoelekeza wabunge wapatikane kwa uwiano.
Ibara hiyo inaeleza kuwa, Bunge la Taifa kutoka kila nchi mwanachama litachagua wabunge tisa kutoka nje ya wabunge wa bunge husika kuwa wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia uwiano wa vyama vya siasa, jinsia na makundi mengine.
Komu pia alikuwa akitaka tafsiri ya kisheria kama taratibu zilikiukwa Spika kumpitisha, John Chipaka kutoka chama cha Tadea kugombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki, hali ya kuwa chama chake hakina mbunge hata mmoja.
Pia Komu alitaka kujua kama ni halali chama ambacho ndiyo kikuu cha upinzani nchini, kinachounda baraza kivuli la mawaziri, kukosa uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki.
Katika uamuzi wa majaji wa mahakama hiyo, wameamua kuwa uchaguzi huo ulikiuka ibara ya 50 ya kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na upatikanaji wa wabunge wa Bunge hilo.
Uamuzi huo, ulieleza kuwa kanuni za Bunge la Jamhuri, ibara ya tano kifungu kidogo cha tano na cha 12 vilivyotumika katika uchaguzi huo, pia vinapingana na Ibara ya 50 na hivyo kusababisha kutopatikana kihalali wagombea wote wa uchaguzi huo.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji alisema kwa mkataba wa Jumuiya hiyo, wabunge wa Bunge hilo, wanapaswa kuchaguliwa kutokana na uwiano wa wabunge katika Bunge la nchi husika na pia kushirikisha makundi mengine ambayo siyo ya vyama vya siasa.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilieleza haina mamlaka ya kutangaza kutengua ubunge wa wabunge wa Tanzania kwa kuwa shauri hilo, sasa linatakiwa kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu hapa nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya hukumu hiyo, Komu na Wakili wake John Mallya ambaye alikuwa akimwakilisha wakili, Damas Mbogoro, walisema kutokana na uamuzi huo, sasa watapeleka uamuzi huo Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
Wakili Mallya alisema shauri hilo, ambalo tayari lilikuwa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, linatarajiwa kutajwa Novemba 27 mwaka huu ili kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa.
“Tuna imani Mahakama Kuu itafuata tafsiri za kisheria zilizotolewa na majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki ili kutangaza rasmi kutengua uchaguzi wa wabunge wa Tanzania,”alisema Mallya.
Hata hivyo, alifafanua kuwa hukumu hiyo, pia imeeleza fursa za Watanzania wengine bila kupitia vyama vya siasa wanaweza kujitokeza kugombea kwa kupitia makundi ya kijamii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni