Kurasa

Alhamisi, 11 Septemba 2014

USIMAMIZI WA MAADILI CBE WAONGEZA UFAULU

Hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) kuendelea kuweka msisitizo katika usimamizi wa maadili kwa wanafunzi imeanza kuzaa matunda kufuatia kuogezeka kwa ufaulu wa masomo kwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho yanayoendelea ya chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965.
Amesema suala la usimamizi wa maadili kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia chuoni hapo limepewa kipaumbele kikubwa na uongozi wake tofauti na miaka iliyopita hali ilinayokifanya chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa vyuo pamoja na taasisi nyingine za elimu ya juu hapa nchini.
“Chuo chetu sasa ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine hapa nchini kwa sababu tumeweza kusimamia suala la maadili hasa uzingatiaji wa mavazi yenye staha kwa wanafunzi hali iliyoongeza heshima kwa chuo chetu”.
Mbali na suala la usimamizi wa mavazi kwa wanafunzi Prof amesema chuo hicho kimeendelea kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia na kutoka katika mazingira ya chuo hicho, kuimarisha ukaguzi katika maeneo yote muhimu ya kuingilia wanafunzi na kuwatambua wanafunzi wote kwa kutumia vitambulisho vyao.
Amefafanua kuwa chuo hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake yakiwemo mabadiliko na maboresho makubwa katika sekta ya elimu hasa ongezeko la udahili wa wanafunzi, ongezeko la fani za masomo na kampasi za chuo hicho katika mikoa mingine nchini ikiwemo Dodoma, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.
Prof. Mjema amefafanua kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo pekee Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.
“Chuo hiki pekee ndicho kinachotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya vipimo, ni chuo kinachotegemewa sana katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki na SADC” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965 na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere , chuo hicho kimepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000 mwaka 2014.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni hapo pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya chuo hicho idadi ya kampasi imeongezeka kutoka 1 ya jijini Dar es salaam na kufikia 4 katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Dodoma na upande wa Zanzibar huku idadi ya wahitimu wa chuo hicho ikiongezeka kwa kipindi chote ikiwa zaidi ya wanafunzi Laki moja.
Aidha, katika kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi katika maadhimisho hayo,chuo kinaandaa matukio mbalimbali ya ukusanyaji wa fedha kupitia chakula cha hisani, matembezi, midahalo ya wasomi na mikutano wanafunzi wahitimu wa chuo hicho Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es salaam kwa ajili ya ujenzi wa maabara, vyumba vya mihadhara ya wanafunzi na madarasa.
Pia chuo hicho kinaandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwajengea uwezo wajasiriamali, na kuwajengea uelewa wanafunzi ili waweze kuwa na uchaguzi sahihi wa hatima yao ya baadaye pindi wanapohitimu mafunzo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni