Kurasa

Ijumaa, 19 Septemba 2014

SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi kudhibiti maandamano yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wafuasi watatu wa chama hicho wamefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam na wengine watano wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro.
Wafuasi hao watano wa mkoani Morogoro wanashikiliwa na polisi wakidaiwa kupinga agizo lilitolewa na viongozi wa jeshi hilo la kuwataka kutoandamana.
Wanachama waliokamatwa ni pamoja na Witnes Makoyola (29), Katibu wa Chadema tawi la Kiwanja cha ndege, Shukuru Makamba(46), Maria Lissu (28) mkazi wa Kilakala na Katibu wa Baraza la Wanawake wilaya ya Morogoro Mjini, Hussein Hassani (28) mkazi wa Mafiga na Odwin Peter (65) mkazi wa Kiwanja cha ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paul alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5:30 asubuhi katika maeneo ya mtaa wa Konga.
Kamanda Paul alisema Septemba 17 viongozi wa chama hicho waliandika barua ya kuomba kuandamana, huku wakidai kuwa lengo la maandamano hayo ni kupinga hatua ya wabunge wa Bunge la Katiba kuendelea na vikao huku wakijua kuwa katiba haitapatikana.
Aidha Kamanda Paul alisema kuwa barua hizo zilienda kwa wakuu wa polisi na kwamba jeshi hilo lilizuia maandamano kutokana na taarifa za kiintelijensia kuwa wapo baadhi ya wananchi walipanga kufanya uhalifu wakati wa maandamano, ikiwa ni pamoja na kuwa kesi ya suala hilo bado iko mahakamani.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema kuwa jeshi hilo liliwaita viongozi wa chama hicho, lengo likiwa ni kuwazuia kuandamana ambapo alisema kuwa jana majira ya saa 5:30 asubuhi katika maeneo ya mtaa wa Konga kulianza kufanyika mkusanyiko wa watu wakijiandaa kuandamana baada ya kuweka ulinzi katika maeneo yote waliyopanga kuanzia maandamano ya wafuasi wa chama hicho.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema walifanikiwa kutawanya mkusanyiko huo kwa kurusha mabomu ya machozi sambamba na kuwakamata watuhumiwa hao ambapo alisema kuwa watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
Kwa upande wake katibu wa chama hicho mkoani hapa, Boniface Ngonyani alisema kuwa maandamano hayo yaliyotarajiwa kufanyika jana majira ya saa 5.00 asubuhi yalizuiwa na jeshi la polisi ambapo jeshi hilo lilidaiwa kuingia ndani ya ofisi za chama hicho na kuanza kupekua nyaraka na kuzitwaa nyingine na kuondoka nazo.
Aidha alisema baada ya hekaheka hiyo baadae wakabaini kwamba kompyuta mpakato ya Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, James Mkude pamoja na simu yake ya mkononi havionekani.
Hata hivyo, alisema kutokana na kukamatwa kwa wanachama hao ofisi ya Chadema mkoa wa Morogoro tayari imewatuma wanasheria wake wawili ili kuweza kufika polisi na kuangalia tatizo lililofanya kukamatwa kwa wanachama hao.
Habari kutoka mkoani Dar es Salaam:
Wafuasi watatu wa Chadema wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuingia katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kinyume na utaratibu.
Wafuasi hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana ni Ngaiza Kamugisha (28) dereva, mkazi wa Vingunguti, Benito Mwapinga (30) Fundi nguo mkazi wa Mtoni kwa Azzi Ally na Eliasante Bugeji (51) Mhasibu wa Hospitali ya CCBRT mkazi wa Komakoma Kinondoni, Dar es Salaam.
Akisoma hati ya mashitaka Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka na George Barasa, ambapo alidai kuwa wafuasi hao wanakabiliwa na mashtaka matatu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kongola alidai mashtaka hayo ni kuingia kwa nguvu Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kukaidi amri halali na kutoa lugha ya matusi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Septemba 18 mwaka huu, washtakiwa waliingia kinyume cha sheria ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa hali ya fujo.
Aidha, ilidaiwa katika tarehe hiyo na maeneo hayo washtakiwa walikataa kutii amri ya halali ya kutawanyika kutoka eneo la makao hayo ya polisi iliyotolewa na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Inspekta Zuhura, ambaye alitoa amri hiyo baada ya kuruhusiwa na viongozi wake.
Akiendelea kusoma mashitaka hayo, alidai katika kosa la tatu linalomkabili Bugeji peke yake, inadaiwa akiwa katika mazingira ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi alitoa lugha ya matusi kwa maofisa wa Polisi. Ilidaiwa maneno hayo yaliyotolewa na mshitakiwa huyo yalikuwa yakiashiria uvunjivu wa amani.
Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na upande wa mashitaka umeomba tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Wakili wa wafuasi hao Peter Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili washtakiwa yanadhaminika, hivyo akaomba mahakama iwapatie masharti nafuu kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Kongola aliendelea kudai kuwa mahakama inatakiwa itoe masharti yanayoendana na mazingira ambayo washtakiwa wametenda kosa hilo.
Kibatala alidai kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhamana ya washtakiwa ni haki yao na pia washtakiwa bado haijawatia hatiani, kwa hiyo dhamana ni haki yao.
Hakimu Moshi alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana wanatakiwa wawe na wadhamini wawili wa kuaminika wakiwemo watumishi wa Serikali au watumishi kutoka katika Taasisi inayotambulika wakiwa na barua za waajili wao na vitambulisho vya kazi na wadhamini watasaini bondi ya Sh 500,000 kwa kila mmoja.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 24 mwaka huu kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na akaamuru washtakiwa warudishwe rumande kwa sababu hawakuwa na wadhamini.
Mpaka mwandishi anaondoka katika eneo la Mahakama washtakiwa walikuwa hawajapata dhamana, ambapo kulikuwa na jitihada za kupiga simu Makao Makuu ya Chadema ili wapate wadhamini.
Nje ya mahakama Mratibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Nickson Tugala alikuwa aking'ang'ania kuingia mahabusu kuwaona washtakiwa, jambo ambalo lilisababisha fujo katika eneo hilo.
Tugala alionekana kubishana na Insepkta wa Jeshi la Polisi, Mussa Mkini mpaka kufikia hatua ya kusogelea kwa karibu hali iliyowatia hofu watu waliyokuwa katika eneo hilo kuwa watu hao wanataka kupigana.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Mkini aombe nguvu kutoka Polisi na ilipofika saa 6:10 mchana ziliingia gari mbili za polisi namba PT 1846 na PT 1145 zikiwa na askari wenye silaha za moto.
Mkini alitoa amri ya Tugala kuchukuliwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na fujo ambazo alikuwa anafanya, lakini bado Tugala alikuwa akiwagomea askari hao.
Baadaye alikubali kuondoka nao, ambapo askari wawili walipanda kwenye gari ambalo alikuwa akiendesha la M4C namba T 351 CAY. Askari mmoja alipanda ndani ya gari na mwingine alipanda nyuma ya gari hilo wakiongoza kwenda Central.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni