Kurasa

Ijumaa, 26 Septemba 2014

MAXIMO AWATAKA WASHABIKI KUFURIKA UWANJANI JUMAPILI

Kikosi cha timu ya Young Africans kitashuka dimba la Uwanja wa Taifa siku ya jumapili kupambana na Wajela Jela timu ya Jeshi la Magereza nchini Prisons FC kutoka jijini Mbeya ikiwa ni mchezo wa pili wa mzunguko wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2014/2015.
Akiongea na tovuti rasmi ya klabu leo mara baada ya mazoezi, kocha mkuu wa Young Africans mbrazil Marcio Maximo amesema vijana wake wako fit kuelekea mchezo huo wa siku ya jumapili huku wakiwa wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu.
Maximo amesema baada ya kupoteza mchezo wa awali dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar, kikosi chake kimekua kikiendelea na mazoezi kila siku katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola huku wakiyafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo wa awali.
Kuhusu timu ya Tanzania Prisons mbrazil Maximo amesema anatambua walishinda mchezo wa awali dhidi ya Ruvu Shooting hivyo wana morali bado ya kuendeleza ushindi siku ya jumapili, lakini pia kikosi changu kipo fit kwa mchezo huo kwa kusaka pointi tatu muhimu.
Aidha Maximo amesema habari njema kwa wana Yanga ni kurejea dimbani kwa kiungo Andrey Coutinho pamoja na mshambuliaji Jerson Tegete ambao wanatarajiwa kuonekana kwenye mchezo huo na kuhakikisha wanaisaidia timu yao kupata ushindi.
Wachezaji watakaoukosa mchezo wa siku ya jumapili ni Oscar Joshua na Hussein Javu ambao wote ni majeruhi, wakisumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, na jumatatu wanatarajiwa kuanza mazoezi mepesi baada ya kuwa kwenye matibabu chini ya usimamizi wa daktari wa timu Dr Suphian Juma.
Mwisho kocha Marcio Maximo amewaomba wapenzi, washabiki, wanachama na wadau wa soka kwa ujumla kujitokeza kwa wingi siku ya jumapili katika mechi dhidi ya Prisons kuja kuwapa sapoti vijana na kuwashangilia muda wote wa mchezo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni