Kurasa

Jumapili, 21 Septemba 2014

DIAMOND ASABABISHA VURUGU UINGEREZA

Mwanamuziki Diamond Platnumz kwa mara nyingine tena usiku wa kuamkia jana alisababisha vurugu kubwa nchini Uingereza baada ya kushindwa kutumbuiza katika ukumbi wa LaFace Club uliopo jijini London.
Hii ni mara ya pili kwa Diamond kusababisha vurugu nchi za ughaibuni baada ya Septemba 1, kusababisha vurugu katika mji wa Stuttgart nchini Ujerumani aliposhindwa kufika kwa wakati ukumbini.
Akizungumza na mwandishi, shuhuda wa tukio ambaye ni Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Uingereza, Flora Lyimo alionyesha wazi kukerwa na tukio hilo ambalo alieleza kuwa huenda likaharibu sifa ya nyota huyo ughaibuni.
Lyimo ambaye alihudhuria shoo hiyo alisema Diamond alisubiriwa na zaidi ya watu 200 tangu saa sita usiku bila nyota huyo kutokea na ilipofika saa 10:00 alfajiri, ndipo walipoanzisha vurugu kudai kurudishiwa pesa zao.
Shoo hiyo ambayo ilitozwa kiingilio cha pauni 20 sawa na fedha za Tanzania Sh54,280 iliishia kwa dosari ya aina yake baada ya polisi kulazimika kuingilia kati kusimamia urudishwaji wa fedha hizo.
Alisema waliamuru watu warudishiwe fedha zao, hivyo walipanga mstari na kurudishiwa fedha zao, kila mmoja akiamuriwa kuondoka eneo hilo huku wenye klabu hiyo wakinyang’anywa leseni.
“Ni jambo la ajabu na aibu kwa msanii ambaye Watanzania tunamtegemea atuwakilishe nje ya nchi anakubali vipi kutangazwa kwenye shoo kama hajalipwa pesa zake, watu wanamchukulia kama tapeli kwani yeye mwenyewe amewatangazia mashabiki wake halafu hajatokea.
“Wengi tunapata shaka kama hajashirikiana na huyo promota kwani hata huo ukumbi ambao shoo ilitakiwa kufanyika hauna jukwaa maalumu ambalo msanii anaweza kutumbuiza binafsi nilishangaa haikuwa eneo sahihi, lakini nikasema ngoja niende kumuunga mkono Mtanzania mwenzangu,”alisema Lyimo.
Hata hivyo, pesa zilizopatikana hazikutosha kuwarudishia watu wote ikizingatiwa kuwa wengi walikata tiketi kabla ya siku ya shoo, hapo ndipo vurugu zilipotokea na polisi kulazimika kumshikilia promota wa shoo hiyo ambaye alifahamika kwa jina la Victor.
“Polisi wengi sana waliofika hapa ukumbini kwa ajili ya kulinda usalama, walichokifanya ni kumchukua promota aliyeandaa shoo hii na kumweka chini ya ulinzi kwa kosa la utapeli, kwa sharti kwamba mpaka watakapompata Diamond, lakini mpaka sasa bado haijajulikana alipo,”alisema Lyimo.
Lyimo alionyesha wasiwasi wake na kueleza kuwa kutokana na mfululizo wa matukio hayo huenda Diamond akazuiliwa kufanya shoo katika nchi za Ulaya, kutokana na kuanza kupoteza imani kwa mashabiki wake.
Mwandishi alimtafuta balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe ambaye alieleza kwamba hafahamu chochote kuhusu tukio hilo na kuahidi kulifuatilia kujua undani wake.
“Kama unasema tukio hilo limetokea usiku mimi sijapata taarifa zozote mpaka sasa, lakini ngoja nijaribu kuwasiliana na mtu ambaye anaweza kufahamu chochote,”alisema Balozi Kallaghe.
Kwa msaada wa Balozi Kallaghe Mwandishi alifanikiwa kuzungumza na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, Rahma Pompy ambaye pia alikuwa kwenye tukio hilo na kufafanua kuwa kasoro hiyo imetokana na uzembe wa promota.
Alisema mwandaaji wa shoo hiyo alitakiwa kumalizana na Diamond kabla ya kuwajaza watu ukumbini, lakini hakufanya hivyo hali iliyosababisha nyota huyo kushindwa kufanya kilichompeleka na kufafanua kuwa hii siyo mara ya kwanza kwa promota huyo mwenye asili ya Tanzania kufanya uzembe wa aina hiyo.
“Kwa mimi niliyekuwepo eneo la tukio nafahamu fika kuwa Diamond hakuwa na kosa lolote, hakulipwa na wala promota hakumfuata hotelini. Unafikiri angeweza vipi kufanya kazi ya namna hiyo,”alisema.
Ingawa mashabiki wengi hawakumwona, lakini Pompy alibainisha kuwa Diamond alifika eneo hilo saa tisa usiku, hata hivyo alishindwa kuingia ndani ya ukumbi huo kutokana na kutomalizana na promota.
“Watu wengi hawakumwona ila mimi nilimwona Diamond, alifika na alionyesha wazi namna alivyokuwa akihangaika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ili kuwaridhisha mashabiki wake, lakini alishindwa kwa sababu hakuwa amelipwa na muda ulikuwa umekwisha,”alisema.
Ilikuwaje Diamond akawasili saa tisa usiku?
Kwa mujibu wa Pompy, baada ya Diamond kusubiri kwa muda mrefu hotelini bila kufuatwa na promota, akaamua kwenda mwenyewe kwenye ukumbi alikotakiwa kufanya shoo. Hata hivyo, alikumbana na usumbufu mkubwa njiani kutokana na barabara nyingi kufungwa nyakati za usiku kutokana na matengenezo.
“Kuna matengenezo ya barabara nyingi zinafungwa, hivyo akajikuta anazunguka kwa muda mrefu kutafuta njia mbadala. Mpaka alivyofika ukumbini, ilikuwa tayari imeshafika saa tisa, hata hivyo asingeweza kufanya chochote kwa kuwa hakumalizana na promota na ukumbi aliotakiwa kufanya shoo unafungwa saa 9:30, nadhani hata yeye alikuwa hafahamu,”alifafanua.
Kuhusu taarifa za Diamond kutafutwa na polisi kutokana na tukio hilo, Pompy alisema hana uhakika na uvumi huo kwa kuwa makosa yalionekana wazi kuwa ni ya promota.
Meneja wa Diamond afunguka
Kutokana na tukio hilo, Meneja wa mwanamuziki huyo, Hamis Taletale maarufu Babu Tale ambaye hakuambatana naye, amesema kuwa Diamond alipokea mwaliko kutoka kwa promota huyo, lakini hakulipwa fedha hata kidogo, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kufanya uamuzi wowote.
“Diamond alipofika Uingereza yule promota alimdaka juu kwa juu kwa kuwa kule alikwenda kwa ajili ya shoo ya Ujerumani itakayofanyika usiku wa leo (jana) akimtaka afanye shoo jijini London, Uingereza, alikubali na baada ya hapo alisema kuwa angemlipa siku ya shoo, lakini kwa wakati wote hakufanikiwa kuonana naye tena, alikuwa akiwasiliana naye kwa simu tu,”anaeleza Taletale.
Alisema Diamond alimsubiri promota huyo kwa muda mrefu, licha ya kufanya matangazo aliamini kuwa kabla muda wa shoo haujafika angemlipa fedha ili aende ukumbini.
“Diamond alishangaa kuona ilipofika saa nne usiku wa kuamkia jana promota yule hapatikani, kwa kuwa hakulipwa hata dola moja (Sh1,600) aliamua kutulia hotelini kwani promota ndiye anatakiwa amfuate msanii, na yeye hakufanya hivyo wala hakumlipa hata kidogo. Msanii wangu hana makosa ndiyo sheria ya kazi ilivyo,”alisema Taletale.
Hata hivyo, Taletale alisema wamiliki wa ukumbi ndio walioamua kuita polisi baada ya kuona viashiria vya vurugu, na hapo ndipo ilipogundulika kuwa promota huyo hakulipia ukumbi pia.
“Licha ya kwamba hakumlipa msanii wangu, pia ukumbi hakuulipia. Alichokifanya mmiliki ni kurudisha fedha kwa watu waliohudhuria mbele ya polisi na promota yule akakamatwa.”
Akizungumzia usalama wa Diamond, Taletale alisema,“Msanii wangu yupo katika mikono salama na hivi tunavyoongea ameshapanda ndege kuelekea Ujerumani kwa ajili ya shoo jioni ya leo. Hana kosa lolote, hakuna mkataba baina yake na promota unaoonyesha kwamba alilipwa,hivyo hakuwa na kizuizi na polisi hawajashughulika naye,”alisema Taletale.
Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini anamwacha msanii wake asafiri peke yake na kufanya makubaliano na mapromota kazi ambayo alitakiwa aifanye yeye (Taletale) alisema:
“Ilikuwa nisafiri naye, lakini kwa bahati mbaya kulikuwa na matatizo ya kifamilia ambayo ilinilazimu nibaki nchini. Yeye alikwenda kwa ajili ya shoo mbili zilizofanyika Jumamosi Afronation na hii ya leo itakayofanyika Sturtgart. Huyu promota alimdaka tu,”alisema Babu Tale.
Baada ya kutokea kwa vurugu hizo, mwanamuziki Diamond alisema promota huyo amemtapeli kwa kuwa hayakuwa makubaliano yao awali.
“Tafadhali ndugu zangu wa Uingereza haikuwa dhamira yangu, kuweni makini sana na promota huyu Victor Dj Rule, mnaposikia kaandaa shoo, pati au hafla yoyote ni vyema kuziepuka na kutohudhuria kabisa kwa sababu ni tapeli, si unajua aisifiaye mvua imemnyeshea, basi miye nimeloa kabisa,”aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Akizungumzia sakata hilo, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba alisema tatizo alilopata Diamond limepokewa kwa masikitiko makubwa na wanamuziki wote nchini.
“Tunasikitika kwani hii ni mara ya pili inatokea tena kwa kipindi cha mwezi mmoja, lakini baada ya kufanya mawasiliano, tumegundua tatizo lilikuwa la promota, mwanamuziki wetu hana hatia na ameshaondoka Uingereza leo (jana) asubuhi na sasa yupo Ujerumani kwa ajili ya shoo nyingine ya usiku wa leo,”alisema Ado.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni