Kurasa

Alhamisi, 3 Julai 2014

KUHUSU VIJANA WATATU WANAODAIWA KUFA KUTOKANA NA KUFANYIWA UKATILI JKT.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limekanusha taarifa zilizosambazwa kuwa vijana wa mujibu wa sheria, wanaoendelea na mafunzo katika kambi za JKT, kuwa wanakufa kwa ukatili.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Erick Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema taarifa hizo potofu zimesambazwa kwa njia ya Ujumbe Mfupi wa Maneno (SMS) katika simu za mkononi na mitandao ya kijamii na zilidai kuwa Kambi ya JKT Oljoro Arusha kuna vijana watatu wamefariki.
Komba alisisitiza kuwa taarifa hizo si za kweli na ni upotoshaji kwa vijana wa Tanzania, kwani ukweli ni kwamba kijana mmoja pekee aliyejulikana kama Honorata Oiso, alifariki katika kikosi cha JKT Oljoro Arusha, kwa ugonjwa wa upungufu wa damu (anaemia), uliosababishwa na malaria na sio watatu kama ilivyoelezwa.
"Wazazi wa kijana aliyefariki walithibitisha kuwa kijana wao alikuwa na matatizo ya upungufu wa damu na sio ukatili, kama ilivyoelezwa na ujumbe uliokuwa ukitumwa kupitia mitandao ya kijamii,’’alisema Komba.
Alisema watu hao wameamua kutumia kifo cha kijana huyo, kusambaza uongo ambao haukubaliki katika jamii.
“Jeshi linasisitiza kuwa hakuna ukatili unaofanywa kwa vijana wanaoendelea na mafunzo katika kambi za JKT,”alisema.
Kwa mujibu wa Komba, hivi sasa JKT lina vijana 38,634 wanaoendelea na mafunzo. Kati yao ni wasichana waliopelekwa kwa mujibu wa sheria ni 5,446 na wavulana 12,822. Kwa upande wa wanaojitolea, wavulana ni 15,509 na wasichana 4,859.
Ofisa Habari wa JKT, Meja Emmanuel Muruga alisema hakuna mwanafunzi anayefanyiwa vitendo vya ukatili na wanafunzi wote waliojiunga kwa mujibu wa sheria, wanapimwa afya kabla ya kuanza mafunzo.
Aliongeza kuwa hata kama mtu atakuwa na ulemavu na ameenda kwa mujibu wa sheria, atafanya mazoezi kama kawaida na kama ana tatizo la afya, kama kifua na mengine, atatembea na wenzake wakikimbia, ila lazima ajumuike na wenzake.
Pia, alisema kwa wale wa kujitolea, kabla ya kujiunga ni lazima wafuate masharti ya JKT. Masharti hayo ni anapaswa kuwa na miaka 18-23, awe mtanzania na asiwe amewahi kuhusika na tukio lolote la uhalifu na akubali mwenyewe kujiunga na jeshi.
Alisisitiza kuwa JKT inalaani kitendo hicho na itafuatilia ili kubaini chanzo chake, na atakayebainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Alisema Jeshi hilo linawakumbusha vijana kuwa makini na matumizi mabaya ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii, hasa taarifa zinazohusiana na jeshi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni