Kurasa

Jumamosi, 26 Julai 2014

HOSPITALI YA IMTU YAFUNGIWA BAADA YA SAKATA LA VIUNGO

Baadhi ya viungo vya miili vilivyokutwa
Oliver Oswald na Adam Malinda, Dar es Salaam
SERIKALI imeifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Tiba na Teknolojia (IMTU) kilichopo Mbezi eneo la Interchiki kwa muda usiofahamika.
Hospitali hiyo imefungiwa kutokana na kukosa sifa, ambapo imebainika kuwa maabara pamoja na wauguzi wake hawana vigezo vya kutoa huduma za kitabibu.
Hatua ya kuifungia hospitali hiyo imekuja siku chache tangu chuo hicho kilipokumbwa na tuhuma nzito za kuhusika na utupaji wa viungo vya binadamu katika eneo la Bonde la Mto Mpiji, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema Serikali imechukua uamuzi huo baada ya kugundua kasoro nyingi zinazoikabili hospitali hiyo.
Alisema katika ukaguzi uliofanywa na jopo la wataalamu kutoka wizarani kwa kushirikiana na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni, ulibaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kuendesha huduma za kitabibu.
“Kweli nimepokea taarifa za kufungiwa kwa Hospitali ya IMTU kutoka katika jopo letu lililokwenda kufanya uchunguzi hospitalini pale ambao wana wajibu wa kutembelea hospitali zote zilizopo ndani ya halmashauri yao kila mara.
“Katika uchunguzi wao wamethibitisha kukuta mapungufu hayo pamoja na mengine ambayo wizara itayaweka wazi katika mkutano wake na waandishi wa habari kesho (leo),” alisema Mwamwaja.
Aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyogunduliwa na jopo hilo kuwa ni pamoja na hospitali hiyo kutokuwa na maabara inayojitosheleza kwa shughuli mbalimbali za kujifunzia pamoja na baadhi ya wauguzi wake kukosa sifa ya kutoa huduma za kitabibu.
Katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi ilibainika kuwa Chuo Kikuu cha IMTU kilihusika na tuhuma za kutupa mabaki ya viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa Julai 22, mwaka huu katika Bonde la Mto Mpiji.
Katika tukio hilo jumla ya mifuko 85 yenye viungo vya binadamu vilivyokaushwa na kuchunwa ngozi viliokotwa, ambapo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwatia nguvuni watumishi wanane kwa kuhusishwa na tukio hilo.
Viungo vilivyookotwa katika eneo hilo ni pamoja na mafuvu ya vichwa, sehemu ya kifua cha binadamu, miguu, mikono, moyo na mbavu.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya wanafunzi wa udaktari wa IMTU, Meekson Mambo, ameelezea kusikitishwa na uamuzi huo wa Serikali, akisema umewaathiri wanafunzi.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana muda mfupi kabla ya gazeti hili halijaenda mtamboni, Mambo alisema kufunga hospitali hiyo ni sawa na kufunga chuo kwa kuwa mafunzo ya vitendo hufanyika katika hospitali hiyo.
“Sisi tunaonewa katika sakata hili kwa kuwa waliofanya uzembe ni viongozi, hatuhusiki kwa namna yoyote na utupwaji wa mabaki ya miili hiyo iliyokutwa huko Mpiji. Kwa kweli uamuzi huu haukuzingatia athari tutakazozipata,” alisema.
Mambo alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuwa makini katika uamuzi inaoufanya, kwani wanafunzi wamebakiza muda mfupi kabla ya kuanza kwa mitihani ya kumaliza mafunzo.
Rais huyo alisema uamuzi huo wa Serikali haukuzingatia umuhimu wa wanachuo kupata haki ya masomo na mafunzo kwa njia ya vitendo, hivyo utawaathiri kisaikolojia.
“Tumebakiza muda mfupi, Agosti 4 mwezi ujao tunaanza mitihani, kama hospitali imefungwa hatima yetu ya mitihani itakuwaje, hii ni kujenga mazingira ya kufanya vibaya katika mitihani yetu,” alisema.
Hata hivyo, Mambo alishauri waliohusika na sakata hilo wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria ili kulinda heshima ya taaluma bila kuathiri wasio husika hasa wanafunzi waliopo chuoni hapo.
Mtanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni