Kurasa

Jumapili, 1 Juni 2014

JAMAA AUA MKE KWA WIVU WA MAPENZI

Mbeya. Watu wanne wamefariki dunia katika matukio tofauti likiwamo la mwanamke mmoja kudaiwa kuuawa na mume wake kutokana na wivu wa mapenzi.
Katika tukio la kwanza, Mkazi wa Kijiji cha Liwalanje, wilayani Mbozi, Christina Hayola (35) amefariki dunia baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kifuani na miguuni na mtu anayedaiwa kuwa mume wake.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba chanzo cha mauaji ni wivu wa mapenzi na kwamba polisi wanamsaka mhusika.
Katika tukio la pili, Msangi alisema mkazi wa Isanga jijini hapa, Abdi Sanga aliuawa kwa vipigo baada ya kutuhumiwa kuwa wizi katika eneo la Forest.
Alisema marehemu anadaiwa alikuwa na mwenzake ambaye alitoroka baada ya kuiba vitenge vyenye thamani ya Sh70,000.
Katika tukio la tatu na la nne, alisema mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ibumila wilayani Mbarali, Fitina Mwandosya alifariki dunia baada ya kudondoka kutoka kwenye trekta dogo aina ya ‘Powertiller’ alilokuwa amepanda akitoka kuvuna mpunga.
Alisema mwanafunzi huyo alipatwa na mkasa huo juzi wakati wanarudi na wenzake waliokwenda kuvuna mpunga wa shule.
Wakati huohuo mwanafunzi mwingine wa kidato cha pili Sekondari ya Makongorosi, wilayani Chunya, Aden Ngombe(17) amefariki dunia juzi baada ya kugongwa na lori aina ya scania alipokuwa akikatisha barabara.
Msangi alisema polisi walimkamata dereva wa lori na kubainika alikuwa amelewa pombe.
Katika matukio mengine watu wanne wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za kukutwa na bastola kinyume na sheria.
Kamanda wa polisi alisema aliyekamatwa na bastola ni mkazi wa Kijiji cha Itentula, Mbozi aliyekuwa na bastola aina ya Baby. risasi tatu.
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni