Kurasa

Jumapili, 8 Juni 2014

BINTI WA MIAKA KUMI NA NANE(18)ABEBWA NA KUVALISHWA NEPI KAMA MTOTO

Morogoro. Wazazi wa binti mwenye ulemavu wa viungo na akili, Farida Abdalah (18) mkazi wa Lukobe Juu wameiomba Serikali, wasamaria wema na wadau mbalimbali kumsaidia binti yao huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika hospitali ya rufaa na anaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Pia wazazi hao ambao walionekana kuwa na hali ngumu ya kimaisha waliomba msaada wa kupatiwa matibabu ya viungo na akili kwa binti yao ili aweze kutembea na kujitambua, kwani kwa sasa binti huyo amekuwa akilala tu kitandani.
Maisha ya binti huyo ambaye umri wake haulingani na umbo lake yameguswa na watu wengi, kwani amekuwa haongei, halii, hasikii na wala hajitambui hivyo amekuwa akivalishwa nepi na kubebwa kama mtoto mchanga.
Akitoa historia ya binti huyo kwa mwandishi wa habari hizi jana mama mzazi wa binti huyo Mwajuma Abdalah alisema kuwa Farida alizaliwa mwaka 1996 wilayani Muheza mkoani Tanga na alijifungulia nyumbani.
Mwajuma alisema kuwa baada ya kuzaliwa binti yake hakuweza kulia na siku zilivyozidi kwenda alimuona akiwa na dalili za kutokuona wala kusikia na ndipo alipompeleka katika kituo cha Afya cha Sabasaba kilichopo Manispaa ya Morogoro ambako aliambiwa kuwa mtoto wake anasumbuliwa na tatizo la mtindio wa ubongo.
“Nimehangaika sana na mtoto wangu baadaye niliamua kumpeleka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambako alianzishwa mazoezi ya viungo, lakini hakuwa na dalili zozote za kupona na kutokana na hali ngumu ya maisha nilishindwa kuendelea na matibabu katika hospitali nyingine kubwa na hivyo nikakata tamaa na nikamshukuru Mungu,” alisema Mwajuma huku akitokwa na machozi.
Hata hivyo alisema kuwa binti yake pamoja na kuwa na ulemavu amekuwa akisumbuliwa na magonjwa mara kwa mara, ukiwamo malaria na kifafa. Kutokana na hali ngumu ya maisha mtoto huyo amekuwa akikosa vyakula bora na hivyo kusumbuliwa na utapiamlo.
Baba mzazi wa binti huyo ambaye naye anasumbuliwa na ugonjwa wa kiuno, Abdalah Musa alisema kuwa hali yake ya maisha kwa sasa imekuwa ngumu sana kwani hana kazi ya kudumu wala biashara na hivyo siku nyingine amekuwa akikosa hata pesa za kumpeleka hospitali binti huyo anapoumwa.
Naye mwenyekiti wa Mtaa wa Lukobe Juu, Joseph Kamanga alisema kuwa taarifa za mtoto huyo alishazifikisha katika Baraza la Maendeleo la Kata na kwa wadau mbalimbali lakini hakuna msaada wowote aliowahi kuupata.
Awali maofisa polisi kutoka dawati la jinsia walipopata taarifa kuhusu ulemavu wa binti huyo, walikwenda kukagua mazingira ya chumba alichokuwa amelazwa na kuridhika kuwa alikuwa akitunzwa vizuri na wazazi wake isipokuwa kutokana na hali ngumu ya maisha baadhi ya mahitaji ikiwamo lishe na matibabu alikuwa akiyakosa.
Hata hivyo waliwasiliana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii na kumchukua binti huyo na kumpeleka hospitali ambako anaendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya yake na kupatiwa matibabu.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoani hapa, Rita Lyamuya alisema kuwa baada ya kupata taarifa za kulazwa kwa mtoto huyo katika hospitali yake amewatuma madaktari kufuatilia kwa karibu afya ya binti huyo na kupata historia kutoka kwa wazazi wake kuanzia mimba hadi makuzi.
MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni