Kurasa

Jumapili, 25 Mei 2014

MZINDAKAYA AGOMA KUMSAMEHE ADUI YAKE KANISANI


Mbunge wa zamani wa jimbo la Kwela, Mzee Chrisant Mzindakaya amekataa kumsamehe hadharani Mbunge wa sasa wa Sumbawanga Mjini, Bw. Aeshi Hilali baada ya kupewa fursa ya kushikana mikono jukwaani na kusameheana.
Haya yametokealeo mchana (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Mzee Mzindakaya alikataa kufanya hivyo akisema yeye ni mkristu lakini hakuwa ameandaliwa kiroho kwa ajili ya tukio hilo. “Hapa ni shughuli ya kanisa na si mkutano wa Chama. Lazima niwe mkweli leo sijajiandaa kwa jambo hili… Mimi ni mtu mzima, nafsi ya msamaha inahitaji maandalizi, nahitaji maandalizi ya kiroho,” alisema.
Hata hivyo, alikiri kwamba amekubali msamaha alioombwa na Bw. Aeshi lakini hawezi kuutoa katika shughuli ya Kanisa. “Nilishamwambia Mwenyekiti wa CCM mkoa aitishe mkutano, wazee wa chama wawepo na sisi wawili tuwepo kwa sababu nimetukanwa sana kama vile sijaifanyia jambo lolote nchi hii,” alisisitiza.
“Niliwaeleza pia waandae mikutano ya nje kule kwa wanachama ambako nilichafuliwa sana. Nikisema nimemsamehe hapa nitakuwa mnafiki,” aliongeza.
Kwa upande wake, Bw. Aeshi ambaye alipewa nafasi ya kwanza kuomba msamaha, alisema anatambua kwamba bega haliwezi kukizidi kichwa na yeye kama mtoto anamuomba msamaha Mzee Mzindakaya kwa yaliyopita ili waweze kufanya kazi pamoja na kuleta maendeleo kwa wakazi wa jimbola Sumbawanga Mjini.
“Natambua kuwa mimi ni mtoto na siku zote mdogo atabaki kuwa mdogo lakini naomba busara zake ili tushirikiane kuleta maendeleo ya mkoa wetu… yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Nimetamka maneno haya mbele ya viongozi wa dini na mbele ya Mungu kwa kuwa najua yuko hapa,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya ndiye aliwaomba Mzee Mzindakaya na Bw. Aeshi wapande jukwaani na kupeana mikono na kisha akawapa kila mtu fursa ya kutoa neno.
Mhandisi Manyanya alisema siku ya leo ni ya kipekee na akaona asipoteze fursa hiyo bali aitumie kuwaomba viongozi hao ambao wamekuwa na uhasama wa muda mrefu wayamalize kwa kupeana mikono hadharani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni