Kurasa

Jumamosi, 10 Mei 2014

MGOMO WA WALIMU WASAIDIA KUWAPA MASLAHI.

MAANDAMANO yaliyofanywa na walimu wapya jijini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita wakidai mishahara na marupurupu mengine yameanza kuzaa matunda, baada ya uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kukubali kuwakopesha sh 200,000 kila mmoja wakati madai yao yakishughulikiwa.
Taarifa ilitolewa na Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT) Wilaya ya Nyamagana, Asha Juma kwa gazeti hili, ilieleza kikao cha uongozi wa halmashauri ya jiji na wawakilishi wa walimu wapya juzi walikubaliana kuwa ni vema wakakopeshwa fedha kidogo kwa ajili ya kujikimu.
“Ni kweli walimu waligoma kuingia madarasani na wakaamua kuandamana wakidai mishahara yao ya mwezi uliopita (Aprili), limepatiwa ufumbuzi jana (juzi) baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kukubali kuwakopesha walimu hao sh 200,000 kila mmoja” alisema.
Alisema baadhi ya nyaraka zilizowasilishwa na walimu hao wizarani zina kasoro ambazo zimesababisha taratibu za kuingizwa kwenye mfumo maalumu wa mishahara ya watumishi wa serikali kuchelewa.
Alifafanua kuwa ni walimu 17 wa sekondari hadi sasa hawajawasilisha vyeti vyao na kungeza kuwa sula la kucheleweshewa mishahara limechangiwa pia na walimu wenyewe kutotimiza masharti ya ajira.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Halifa Hida alikiri kuwepo kwa makubaliano pamoja na mapungufu yaliyojitokeza.
VIA TANZANIA DAIMA.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni