Kurasa

Jumanne, 20 Mei 2014

BAADA YA KUJUA KUWA MENEJA EWURA ALIJINYONGA POLISI SASA KUCHUNGUZA SABABU

Dar es Salaam.Aliyekuwa Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza alijinyonga kwa tai. Taarifa iliyotolewa jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Engelbert Kiondo imesema.
Baada ya taarifa hiyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeunda jopo kuchunguza sababu za kifo hicho.
Meneja huyo alikutwa amekufa katika Gesti ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo na kifo chake kinaelezwa kutokea katika mazingira ya kutatanisha. Alijinyonga muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Dodoma ambako alihudhuria mkutano kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa jopo hilo litaongozwa na Mkuu wa Upelelezi kanda hiyo, Jaffary Mohamed atakayeshirikiana na wataalamu wa Maabara Kuu ya Polisi, daktari bingwa wa Polisi na serikalini.
Kova alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi ili kuondoa utata ulioanza kujitokeza kuhusiana na kifo chake baada ya taarifa kuzagaa kwamba kilitokana na kutoelewana na viongozi wenzake katika masuala ya kikazi.
Alisema uchunguzi huo ukikamilika, jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Kinachofanyika ni kupata maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa shughuli za marehemu na hali iliyomsibu kabla ya kifo chake kwani hakuacha ujumbe wowote wa maandishi au wa mdomo,” alisema Kova.
Alisema maelezo mbalimbali ya mashahidi yanaendelea kuchukuliwa ili kufahamu kama kuna kosa la kijinai, kiutawala au yote.
Kamanda wa Mkoa wa Temeke
Kamanda Kiondo alisema: “Uchunguzi ninaoufahamu hadi sasa ni kuwa Gashaza alijinyonga kwa kutumia tai yake, akiwa bafuni katika hoteli ya Mwanga. Alitumia stuli kupanda juu, stuli ilianguka na tai ilikatika ndipo mauti yakamfika,” alisema.
Alisema mwili wake ulionekana kuvimba kutokana na kujinyonga na inaonekana mshipa wa hewa ulizibwa na kusababisha kifo chake.
Kamanda Kiondo alisema kutokana na kuthibitika kuwa Gashaza amejinyonga, uchunguzi utakaofanyika ni kujua chanzo cha kujinyonga.
VIA:MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni