Kurasa

Ijumaa, 18 Aprili 2014

MMEKIMBIA LAKINI VIKAO VITAENDELEA.

Licha ya baadhi ya wabunge wa Upinzani wa Bunge Maalum la Katiba kuamua kususia kuendelea kushiriki katika mjadala wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa ndani ya Bunge hilo Kundi kubwa la Wajumbe hao waliobaki wataendelea kuchapa kazi waliyotumwa na Wananchi bila ya kujali uwamuzi uliochukuliwa na wale walioamua kutoka nje ya mjadala huo.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mbunge wa Bunge hilo Maalum la Katiba Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kutembelea baadhi ya Mabanda ya Maonyesho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es salaam ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya kutimia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964.
Balozi Seif alisema Kundi hilo lililobakia ndani ya Bunge hilo halitatetereka kamwe na litatekeleza wajibu wake na lina uwezo kamili wa kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Bunge hilo Maalum la Katiba na baadaye kuipeleka kwa Wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea masikitiko yake na kuvunjwa moyo kutokana na kitendo hicho kilichoibuka ndani ya Bunge hilo ambacho hakionyeshi uungwana wala uvumilivu na kinaonyesha muelekeo wa kuwanyima haki ya Kidemokrasia Watanzania.
“ Kundi lililobakia ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni kubwa na lina uwezo wa kutekeleza kazi hiyo muhimu katika Historia ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zetu tulizojipangia kwa pamoja sisi na wale walioamua kuukimbia mjadala huo “. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia suala la Muungano wa Tanzania kutimia miaka 50 tokea kuasisiwa kwake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Muungano huo umeleta faida kubwa kiasi kwamba Watanzania walio wengi wamenufaika nao Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.
Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeongeza kuleta upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi wa pande zote mbili na kuupa fursa kubwa zaidi Zanzibar katika kupanua wigo wa Kibiashara sambamba na umiliki wa maeneo makubwa ya ardhi kwa Wazanzibari walio wengi ambao kwa muda mrefu hivi sasa wanaendelea kuishi upande wa Tanzania Bara.
Balozi Seif alitanabahisha kwamba kwa vile Muungano wa Wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara ni wa asili ni vyema kwa watu wa pande hizo mbili wakaendelea kuuenzi na kuuimarisha kwa faida ya vizazi vya sasa na vile vijavyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi ulioandaa na kusimamia Maonyeso hayo ya kutimia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa juhudi kubwa walizochukuwa na hatimae kufanikisha vizuri Maonyesho hayo.
Alisema Maonyesho hayo yamependeza kiasi kwamba wananchi wengi wamevutiwa nayo na kushawishika kutembelea kwa lengo la kujifunza na kuona bidhaa na harakati za kiutendaji za Taasisi na Mashirika ya Sekta za Muungano yaliyoamua kushiriki kwenye Maonyesho hayo.
“ Maonyesho ni mazuri na yamependeza. Ukweli nimefarajika na maandalizi ya Maonyesho hayo yenye kuonyesha maendeleo makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 50 katika Taasisi na Mashirika ya Sekta mbali mbali za Muungano zinazofanya kazi Zanzibar na Tanzania Bara“. Alifafanua Balozi Seif. Balozi Seif aliwaomba Wananchi mbali mbali Nchini kuangalia Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kupitia Maonyesho hayo ili wapate fursa kamili ya kujifunza kwa undani Historia hiyo.
Alisema hatua hiyo muhimu itasaidia kuwapa nafasi nzuri ya kuelewa ukweli na kujiepusha na watu na makundi yenye tabia ya kuendelea kuupotosha umma juu ya historia halisi ya Muungano huo unaoendelea kuwa kielelezo kikubwa katika Nyanja za Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akifuatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa { TAMISEMI } Nd. Zubeir Sarataba alipata wasaa wa kutembelea baadhi ya Mabanda yaliyoshiriki kwenye Maonyesho hayo. Miongoni mwa Mabanda hayo ni pamoja na lile la Nguvu za Atomiki,Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na Mambo ya Nje na Ushirikiano na Kimataifa. Mengine ni Banda la Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka ya Kodi ya Ongezeko la thamani { TRA } pamoja na Banda la Mahakama ya Tanzania ambapo alibahatika kujionea hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Taasisi hizo kupitia maonyesho hayo. Jumla ya Mabanda 50 ya Mashirika na Taasisi mbali mbali za Sekta za Muungano zinazofanya kazi pande zote mbili za Muungano Bara na Zanzibar zimeshikiri kwenye Maonyesho hayo ya kutimia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni