Kurasa

Jumatatu, 28 Aprili 2014

HEBU SOMA MKASA HUU WA MZEE ALIEKATWA NYETI KAMA ANAVYOSIMULIA MWENYEWE.

Mbeya. Aprili 19, Mzee London Haonga (61) alipatwa na tukio la kutisha kwa kukatwa sehemu zake za siri. Ni tukio la kusikitisha ambalo linadaiwa kufanywa na vijana wadogo.
Haonga alipatwa na masahibu hayo akiwa nyumbani kwake Kijiji cha Mapogolo wilayani Ileje. Majirani walisikia yowe kutoka kwa mzee huyo na kufika eneo la tukio, lakini walikuwa wamechelewa kwa kuwa wahalifu hao walikuwa tayari wameshatokomea na viungo vya siri kwa mzee huyo.
Hata hivyo, majirani hao walimbeba mzee huyo hadi Hospitali ya Wilaya ya Ileje ambako alihamishia Hospitali ya Rufaa Mbeya alikolazwa mpaka sasa.
Akizungumza na gazeti hili akiwa Wodi 1, Haonga anasema tukio hilo kwake lilikuwa la kinyama na ukatili kwani wahusika walimchinja bila huruma na kumsababishia maumivu makali ambayo yalisababisha apoteze fahamu.
“Ilikuwa Jumamosi saa 8.00 mchana alipokuja mjukuu wa kaka yangu nyumbani kwangu na kunieleza kuwa alitumwa kuja kuchukua dawa ya kizunguzungu. Nilimjibu kuwa sina dawa hiyo hapa ndani hadi niende kutafuta porini. Hivyo tukakubaliana kuwa atakuja jioni kuchukua dawa,” anasema mzee huyo ambaye ni mtaalamu wa dawa za asili.
Anasimulia kuwa ilipofika saa 2:30 usiku alifika kijana huyo na akampa dawa hiyo. Alipotaka kuondoka alimwomba amsindikize na akampa fimbo kwa ajili ya kujilinda njiani kwa kuwa nje kulikuwa na giza nene.
“Tulipotoka nyumbani, tukiwa mbali kidogo na nyumbani kwangu, ghafla akanifunika usoni na kofia aliyokuwa amevaa na kunikaba shingo huku akiniambia kuwa ‘Wewe mzee leo utaona,’ baadaye akaniangusha chini,” anasema.
Akisimulia huku akionyesha kujisikia maumivu makali, Haonga anasema baada ya kuanguka chini, aligundua kuwa mjukuu wake hakuwa peke yake.
“Walikuwa zaidi ya watu wawili kwa kuwa nikiwa nimezibwa uso na kofia na kukabwa shingo, mwingine alinimvua suruali,” anakumbuka.
Anasema kuwa baada ya muda mfupi alipoteza fahamu na alizinduka akiwa wodini Hospitali ya Rufaa na kuelezwa na wauguzi na madaktari kuwa sehemu zake za siri zimeondolewa na kubakia kidonda ambacho anaendelea kupatiwa matibabu.
Mzee Haonga anasema kuwa bado hali yake siyo nzuri kwani maumivu anayoyapata ni makali na kwamba maumivu mengine anayapata katika sehemu ya shingo na kifua.
Anasema kuwa nyumbani kwake anaishi peke yake katika kipindi cha miaka minne kutokana na kufiwa na wake zake wawili na kubakiwa na watoto ambao wote wanajitegemea, hivyo anaamini watu hao walitumia nafasi hiyo ya kumlaghai na kumfanyia unyama huo .
CHANZO:MWANANCHI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni