Kurasa

Alhamisi, 17 Aprili 2014

CHAMA CHA WAFANYAKAZI CHAANZA KUITIBUA SERIKALI.

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limebaini kuwa wafanyakazi wengi nchini bado wanakabiliwa na maisha magumu kutokana na malipo duni ya ujira.
Pia limesema kutozingatiwa kwa sheria za kazi, uchumi usio imara, kukosekana kwa utashi wa kisiasa na vikao vya majadiliano visivyo na tija ndiko kunachangia uchumi wa wananchi kudidimia.
Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya, alibainisha hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kufanyika kwa kikao cha 15 cha Baraza Kuu la shirikisho hilo.
Alisema baraza hilo limebaini kima cha chini cha mshahara kwa sekta zote mbili – za umma na binafsi – bado hakijafikia hata sh 315,000 kima ambacho kimekuwa kikidaiwa kwa takribani miaka tisa iliyopita.
“Kima cha chini cha serikali hivi sasa ni sh 240,000 sawa na sh 8,000 kwa siku, waajiri walio wengi katika sekta binafsi wanalipa kati ya sh 100,000 hadi sh 150,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na sh 3,500 na sh 5,000 kwa siku,” alieleza Mgaya.
Alisema Baraza Kuu limebaini ulipaji wa mishahara duni hautokani na kutokuwa na uwezo wa kulipa, bali ni mtindo uliozoeleka wa kutoheshimu nguvu kazi, na kwamba wanaamini nguvu kazi si mojawapo ya vipaumbele vya taifa kwa imani kuwa inapatikana kirahisi na kwa bei rahisi.
“Baraza Kuu pia lilijadili suala la kodi, kwamba licha ya kuwa na malalamiko ya muda mrefu, wafanyakazi wameendelea kubebeshwa mzigo mkubwa wa kodi ya mapato.
“Shirikisho limekuwa likidai kwa muda mrefu kodi ya mapato kwa wafanyakazi iwe chini ya asilimia 10, na kwamba wigo wa walipaji wa kodi hiyo upanuliwe, lakini badala ya serikali kulitazama jambo hili kwa umakini na kitaalamu, imekuwa ama ikiongeza kima cha mshahara kinachoelezwa kwamba hakitozwi kodi au kupunguza asilimia moja,” alieleza Mgaya.
Pia alisema Baraza Kuu lilizungumzia pensheni ambapo limebaini maboresho ya hifadhi ya jamii yaliyokuwa yakisimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), bado hayajasaidia kutatua kero ya muda mrefu ya malipo duni ya pensheni.
Katika hatua nyingine, Mgaya amekiita kikundi cha watu watano kinachompinga kuwa ni cha chuki binafsi za kiungozi, kwa kuwa walishindwa katika uchaguzi wa nafasi aliyonayo.
Alisema kikundi hicho cha watu watano ambao walizungumza na vyombo vya habari wakidai kuwa hawamtaki kwa kuwa ana umri mkubwa, matumizi mabaya ya fedha, kutosimamia vizuri kitega uchumi, kinafanya hivyo kutokana na sababu binafsi za kushindwa katika nafasi hiyo ya ukatibu mkuu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni